Spika wa Baraza la Wawakilishi apokea Vitabu vya Ripoti ya CAG ya mwaka 2021/2022
Posted on: 12.05.2023
Spika wa Baraza
la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Zubeir ali Maulid amepokea vitabu vya Ripoti ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2021/2022 na kusema kuwa ripoti
hizo zitaanza kufanyiwa kazi haraka ili ziweze kutoa mapendekezo
yanayohitajika.
Mhe Zuberi
akipokea vitabu saba vya Ripoti hizo kutoka kwa Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Katiba,
Sheria na Utawala bora Mhe. Haroun Ali Suleiman amesema Ripoti hizo
zitakabidhiwa katika kamati za Baraza la Wawakilishi zinazohusika na masuala ya
uchunguzi wa hesabu za Serikali ili ziweze kufanyiwa kazi na baadae kuweza
kutolewa ufafanuzi wa yale yaliyofichuliwa ndani ya ripoti hizo.
Waziri wa Nchi
Afisi ya Rais Katiba, Sheria na Utawala bora Mhe Haroun Ali Suleiman amesema Ripoti
alizowasilisha ni pamoja na taarifa ya Serikali kuu, Idara maalum za SMZ, Mifumo
ya Tehama ya SMZ, Mashirika ya umma, Miradi ya maendeleo, Ukaguzi wa kiufundi
na mfuko wa maendeleo ya jimbo na miradi ya maendeleo ya wadi.
Waziri Nchi
Afisi ya Makamo wa Pili wa Rais, sera uratibu na Baraza la Wawakilishi Mhe Hamza
Hassan Juma na Makamo Wenyeviti wa Kamati ya PAC na LAAC wamesema wataendelea
kuzifanyia kazi Ripoti hizo kwa umuhimu wake ili ziweze kuchukuliwa hatua kwa
pale patakapohitajika.
Mwisho