Wakati wa Utawala wa Waarabu
Kwa vile Zanzibar ilitawaliwa na idadi tofauti ya wageni wakiwemo Wareno, Waarabu na Waingereza, historia yake ya Kibunge ilikuwa imeathiriwa na mifumo yao ya asili ya kutunga sheria. Kwa hiyo wakati wa Utawala wa Waarabu, (1832-1920), Nchi ya Zanzibar ilikuwa na mfumo wa kufanya maamuzi (Mfumo wa Kibunge) kwa kupitia Majlis al Shura, ambayo ilitunga sheria kwa kuegemea kwa kiasi kikubwa mamlaka binafsi ya Sultan, kama mtawala mkuu wa wakati huo.
Makubaliano ya kuilinda Zanzibar yaliyotiwa saini kati ya Uingereza na Sultan wa Zanzibar tarehe 14 Juni 1890, yalileta mabadiliko makubwa ya kuiweka Zanzibar chini ya ulinzi wa Uingereza. Na hivyo ilikuwa moja ya mabadiliko makubwa katika historia ya kibunge kutoka Zanzibar ilivyokuwa chini ya mikono ya Waarabu hadi kuwa chini ya mikono ya Uingereza. Hali hiyo iliathiri mwanzo wa historia ya kikatiba ya Zanzibar. Mnamo mwaka wa 1891 Serikali ya Kikatiba ilianzishwa, na Jenerali Sir Lloyd Mathews kama Waziri wa Kwanza wa Uingereza nchini Zanzibar.
Wakati wa Utawala wa Waingereza
Wakati wa utawala wa Waingereza (tarehe 1 Julai 1913), historia ya kutunga sheria ya Zanzibar ilikuwa kwa athari ya kuhamisha mfumo wa utawala wa Uingereza, kutoka “Ofisi ya Nje” hadi “Ofisi ya Kikoloni” na kufuta nyadhifa za “Waziri wa Kwanza” na “Balozi Mkuu ” kwa kuubadilisha na wadhifa mpya wa “Muingereza Mkaazi”, mabadiliko ambayo hayakumfurahisha Sultan (Seyyid Khalifa bin Haroub ambaye alishika kiti cha ufalme mwaka 1911) kwani yalimnyang’anya mamlaka ya kikoloni na kushusha hadhi ya utawala wake
Kutokana na malalamiko ya Sultan, historia ya Kibunge ya Zanzibar ilichukua mabadiliko mengine yanayojulikana kama Baraza la Ulinzi ambalo mwenyekiti wake (kama siku hizi anavyofahamika kwa jina la Spika) alikuwa Sultan kama Rais wakati Muingereza Mkaazi akiwa ni Makamu wa Rais (tunaweza kusema kuwa katika mifumo ya Kibunge ya siku hizi, ni sawa na Naibu Spika). Mabadiliko hayo yalifanyika chini ya Amri ya Kisheria (Decree) ya Baraza la Ulinzi (Amri Na. 6 ya 1914). Amri hiyo ilianzisha zaidi (iliruhusu) wajumbe wengine sita kuwa wajumbe wa Baraza la Ulinzi, wakiwemo wajumbe watatu walioingia kwa nafasi zao (ex-official members) (ambao ni Mwanasheria Mkuu, Mhasibu Mkuu wa Serikali na Mkuu wa Masuala ya Serikali) na wajumbe watatu wasio rasmi waliopendekezwa na Sultan (ambao walikuwa Mwarabu, Muesia, na Mzungu). Baraza hili lilikuwa chombo cha ushauri kwa Sultan Mtukufu.
Mnamo mwaka 1926, Amri ya Sheria ya Mabaraza (Decree) ilipitishwa (Amri Na. 1 ya mwaka 1926) iliyoanzisha Baraza la Kiutendaji (Executive Council) (EXCO) na Baraza la Kutunga Sheria (Legislative Council) (LEGCO). Mabaraza hayo mawili yalikuwa na mamlaka tofauti, mamlaka ya kiutawala yalipewa Baraza la Kiutendaji, ambalo hasa lilikuwa na watawala wakuu wa Uingereza, na Sultan kama Mkuu wa Baraza. Mamlaka ya kutunga sheria yalitolewa kwa Baraza la Kutunga Sheria (LEGCO) ambalo liliongozwa na Muingereza Mkaazi (kama Spika wa chombo hicho), lakini bado mswada uliopitishwa ulikuwa na kibali cha Mtukufu Sultan.
LEGCO ilikuwa na wanachama 12; baadhi yao walikuwa kutoka upande wa Serikali (wajumbe watatu walioingia kwa nafasi zao na wajumbe watatu waliokuwa wajumbe rasmi). Wajumbe wengine sita waliteuliwa kuwa wajumbe mbali na makundi rasmi rasmi. Kwa kipindi cha miaka ishirini ya uhai wa LEGCO, hapakuwa na uwakilishi wa Muafrika. Uwakilishi wa Waafrika katika LEGCO ulianza mwaka wa 1946 wakati Sheikh Ameir Tajo alipoteuliwa kuwawakilisha Waafrika. Mwaka 1947 Sheikh Ali Shariff pia aliteuliwa katika LEGCO kwa lengo la kuongeza uwakilishi wa Waafrika.
Uteuzi wa Waafrika wawili ulisababisha msukosuko wa ubaguzi wa rangi ambapo makundi mengine ya kikabila yalidai uwakilishi wao pia. Hali hiyo ilionekana kutovumilika kwa Muingereza Mkaazi ambaye alilazimika kuongeza uwakilishi wa Waafrika hadi kufikia watu wanne, Waarabu wanne, Waasia watatu na Mzungu mmoja bila kuathiri uteuzi wa wajumbe walioteuliwa kwa nafasi zao.
Mnamo mwaka 1956, Amri mpya ya Sheria (Decree) ilipitishwa, ambayo ilibatilisha Amri iliyotangulia ya 1926. Amri hiyo mpya iliyopitishwa ilianzisha tena Baraza la Kiutendaji na Baraza la Kutunga Sheria pamoja na Baraza la Faragha katika mwaka huo huo. Bwana W.F Coutts ambaye aliteuliwa kushauri mbinu zitakazotumika katika kuchagua wajumbe wasio rasmi wa LEGCO alipendekeza kuwa kati ya wajumbe kumi na mbili wasio rasmi, uchaguzi wa pamoja ufanyike kwa wajumbe sita wasio rasmi, kwa kuzingatia sifa za umri maalum wa kuruhusiwa kupiga kura, sifa za umiliki wa mali na elimu. Pendekezo hilo lilikubaliwa na lilikuwa msingi wa uchaguzi wa mwaka 1957 chini ya utaratibu uliowekwa katika Amri ya Uchaguzi wa Baraza la Kutunga Sheria ya mwaka 1957.
Baada ya hapo, mapambano ya kudai uhuru yalikuwa yakiongezeka katikati ya miaka ya 1950 amabpo vikundi vya ukabila vilibadilishwa kuwa vyama vya kisiasa vilivyodai uhuru. Uchaguzi wa kwanza ulifanyika mwaka wa 1957. Tangu wakati huo wanachama wasio rasmi wa LEGCO walipatikana kutokana na matokeo ya uchaguzi pamoja na wateule wa Sultan.
Amri ya Sheria ya Baraza ya mwaka 1956 lilifanyiwa marekebisho mwaka wa 1960. Marekebisho haya yalikuwa makubwa kwa sababu, kwa mara ya kwanza nafasi za Spika na Naibu Spika zilianzishwa. Hivyo, Muingereza Mkaazi hakuwa tena Afisa Msimamizi wa LEGCO.
Mapambano ya Uhuru na Athari zake
Baadaye, chaguzi nyingine zilifanyika Januari 1961, Juni 1962 na Julai 1963. Chombo kipya cha kutunga sheria cha Zanzibar kilianzishwa kwa Katiba ya wakati huo ya Dola ya Zanzibar ya mwaka 1963 (Decree No. 10 of 1963), ambayo ilikuwa Katiba ya kwanza ya Zanzibar kuanzisha Bunge la Zanzibar ambalo liliitwa Bunge la Taifa. Katiba ilianzisha wadhifa wa Spika na Naibu Spika wa Bunge kwa mara ya kwanza katika historia ya kutunga sheria Zanzibar. Hata hivyo, Katiba hiyo ilidumu kwa muda mfupi wa mwezi mmoja na kufutwa na Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.
Kutokana na mapinduzi ya mwaka 1964, historia ya Chombo cha Kutunga Sheria cha Zanzibar ilibadilika na kuwa enzi mpya za chombo cha kutunga sheria kuwa ni Baraza la Mapinduzi, wakati huo huo kikitekeleza majukumu ya kiutendaji ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Baraza la Mapinduzi lilidumu kwa miaka 16 katika historia ya nchi, hadi mwaka 1980 Baraza la Wawakilishi Zanzibar (HRZ) lilipozinduliwa mnamo tarehe 14 Januari 1980 ikiwa ni zao la Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1979, chini ya kifungu cha 21 cha Katiba hiyo.
Kuanzishwa kwa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar
Mwaka 1984, Katiba ya 1979 ilifutwa na nafasi yake kuchukuliwa na Katiba mpya ya Zanzibar ya 1984. Waraka huu ni halali hadi sasa na umekuwa msingi wa kisheria wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar. Kifungu cha 63 cha Katiba ya 1984 kinatoa uhalali wake. Pamoja na hayo, Ibara ya 106 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (URT) inalitambua Baraza la Wawakilishi la Zanzibar. Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ni taasisi ya uwakilishi wa kidemokrasia kwa wananchi wa Zanzibar. Ina kazi za kutunga sheria, fedha na uwakilishi kwa mambo yote yasiyo ya muungano kwa Zanzibar.