PAC yakagua skuli za mradi wa madarasa 1000 zilizomo katika Ripoti ya CAG.

Posted on: 02.08.2026
PAC yakagua skuli za mradi wa madarasa 1000 zilizomo katika Ripoti ya CAG.
Kamati ya Hesabu za Serikali ya Baraza la Wawakilishi (PAC) imewashauri washauri elekezi wa wizara na taasisi mbalimbali za Serikali kuhakikisha wanasimamia na kuwaelekeza wakandarasi katika miradi ya ujenzi wa majengo mbalimbali ya Serikali.
Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Kombo Mwinyi Shehe imetoa ushauri huo baada ya kutembelea skuli mbalimbali zilizomo katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu ujenzi wa madarasa elfu moja kwa skuli za Zanzibar kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024.
Kamati hiyo imebaini baadhi ya mapungufu katika majengo hayo na kusema kuwa inaunga mkono uamuzi wa Serikali wa kujenga majengo hayo ili kupunguza changamoto ya uhaba wa madarasa hivyo imewashauri washauri elekezi kuwa na uzalendo wa kuzingatia mahitaji na ubora wa miradi ya maendeleo katika kufikia malengo ya Serikali.
Kwaa upande wake Mhandisi wa Wizara ya Elimu Zanzibar Ndg. Khamis Rashid Mtara amesema majengo hayo bado yako imara mbali ya kasoro ndogondogo zilizojitokeza ambazo zinaweza kurekebishika.
Kamati hiyo ilitembelea skuli ya Utaani, Konde na Kojani kwa upande wa Pemba na Skuli ya Chukwani na Makunduchi kwa Unguja.