HOUSE OF REPRESENTATIVES

BARAZA LA WAWAKILISHI

News from the House

RAIS SHEIN AVUNJA BLW

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohammed Shein amewanasihi Wajumbe wa Baraza la Tisa la Wawakilishi kuendelea kutumia maarifa na uzoefu walioupata katika Baraza hilo katika kuongoza na kushiriki kikamilifu katika harakati za kusukuma mbele maendeleo ya taifa.

Rais Dkt Shein ameyasema hayo wakati akitoa hotuba  ya kuvunja  Baraza la Tisa la Wawakilishi huko katika ukumbi wa Baraza hilo Chukwani Mjini Zanzibar.

Amesema  ana imani kuwa Wajumbe hao watakua hazina kubwa  katika kupanga  kushauri na kutekeleza mipango ya kujenga nchi.

Aidha amewanasihi wale ambao wenye nia ya kugombea  na kubahatika  kuchaguliwa  kurejea tena  katika Baraza la Wawakilishi waendelee  kuilinda, kuitii na kuitetea kwa vitendo  katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Pamoja na hayo amempongeza Spika wa Baraza la Wawakilshi Mhe Zubeir Ali Maulid  na wasaidizi wake katika kuliongoza vizuri Baraza hilo kwa kuzingatia haki uadilifu na ufanisi mkubwa katika kukuza demokrasia na utawala bora.

Akizungumzia Uchaguzi mkuu amesema Serikali itaendelea kuhakikisha hali ya amani na utulivu iliopo nchini inaendelea kudumu kabla na baada ya uchaguzi mkuu.

Amesema  Serikali imetunga sheria ya uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018  hivyo ni wajibu wa Viongozi wa vyama vya siasa na wanachama kuheshimu kazi na majukumu ya tume za uchaguzi nchini  [ZEC na NEC.]

Amesema huu ni wakati wa kudhihirisha ustaarabu katika siasa, umoja, mshikamno na utiifu wa sheria zilizopo katika kutekeleza jukumu la kuitunza amani.


Hon. Zubeir Ali Maulid (Speaker)

Upcoming Events

Stay connected