HOUSE OF REPRESENTATIVES

BARAZA LA WAWAKILISHI

News from the House

Bajeti ya SMZ yafikia Trilioni

Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar imepandisha bajeti yake ambapo  kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 imepanda kutoka bilioni 841.5 hadi kufikia Trilioni 1,0874 huku vipaombele katika bajeti hiyo ni kuimarisha ubora wa huduma za kijamii zikiwemo elimu, afya, makaazi na upatikanaji wa maji safi na salama.

Vipaombele vyengine ni Kuimarisha miundombinu ya uingiaji nchini inayojumuisha bandari na viwanja vya ndege,Kuimarisha miundombinu ya msingi ikiwemo barabara, nishati na kuimarisha Utalii.

Akisoma hotuba kuhusu mapendekezo ya bajeti hiyo Waziri wa Fedha na Mipango Dk Khalid Salum Mohammed,alisema utegemezi wa bajeti kutoka kwa wahisani wa maendeleo  unatarajiwa kushuka zaidi na kufikia asilimia 7.3.

Alisema bajeti hiyo ya mwaka huu wa fedha inaashiria mageuzi makubwa ambayo kwa kiasi kikubwa Serikali itakuwa inatumia yenyewe sehemu kubwa ya mapato yake.

Alisema Serikali inatarajia kukusanya mapato ya ndani shilingi bilioni 675.9 na bilioni 380.5 zinatokana na ruzuku na mikopo kutoka nje na bilioni 30.0 za mikopo ya ndani.

Akieleza muelekeo wa mapato ya bajeti hiyo alisema, tayari Zanzibar inaonesha kiwango cha juu cha ukusanyaji wa mapato kulingana na uchumi wake ambapo uwiano wa mapato ya ndani na pato la taifa ni asilimia 22.6 kwa mwaka 2016/2017.

Hata hivyo alisema uwiano wa mapato wa kodi kwa pato la taifa ni asilimia 12 huku jitihada zaidi zinakusudiwa kuwekwa mwaka 2017 kwa uwiyano wa mapato ya ndani kufikia asilimia 23.5 ya pato la taifa wakati mapato yatokanayo na kodi yakifikia asilimia 22.8 ya pato la Taifa.

 


Hon. Zubeir Ali Maulid (Speaker)

Upcoming Events

Stay connected